Gari la matangazo ya moja kwa moja (OB Van) la Azam Media Group limeharibiwa katika Uwanja wa Dandora, jijini Nairobi, wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Kenya kati ya Nairobi United FC na Gor Mahia FC.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Azam Media Kenya Limited, tukio hilo limetokea jana majira ya saa 10:00 jioni wakati matangazo ya moja kwa moja ya televisheni yakiendelea.
Azam Media Group imelaani vikali tukio hilo, ikisema kuwa vitendo vya uharibifu vinahatarisha juhudi za kukuza na kutoa mwonekano wa kimataifa kwa Ligi Kuu ya Kenya kupitia matangazo ya moja kwa moja.
Aidha, kampuni hiyo imesisitiza kuwa inahakikisha usalama wa hali ya juu kwa wafanyakazi wake wa uzalishaji na inaendelea kufuatilia tukio hilo kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF).
Azam Media Group imetaja tukio hilo kama kitendo cha kihuni kinachoipa soka la Kenya taswira mbaya, huku ikiahidi kutoa ripoti kamili mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Comments
Post a Comment